Hatimaye Chelsea wamemfukuza kocha wao, Jose Mourinho aliyependa
kujiita majina ya ajabu kama The Special One, The Only One au The
Happy One.
Hatua hiyo imechukuliwa na mmiliki wa klabu, bilionea wa Urusi, Roman
Abramovich, sababu ikiwa mwenendo mbovu kwenye Ligi Kuu, ambapo
Chelsea wapo nafasi ya 16 baada ya mechi 16 pia wakiwa na pointi 15.
Chelsea waliopoteza matumaini ya kutetea ubingwa huo kutokana na
tofauti ya pointi 20 iliyopo kati yao na vinara Leicester wameondokana
na kocha aliyewaongoza wka mafanikio makubwa na kutwaa ubingwa miezi
saba tu iliyopita.
Mourinho (52) alirejea Chelsea Juni 2013 kwa awamu ya pili, ambapo
msimu uliopita walimaliza ligi wakiwaacha waliowafuatia, Manchester
City kwa tofauti ya pointi nane. Mechi yake ya mwisho ilikuwa Jumatatu
wiki hii ambapo walichapwa 2-1 na Leicester.
Taarifa ya Klabu ya Chelsea iliyotolewa muda mfupi uliopita imedai
kwamba wameamua kuachana kwa maridhiano.
“Wote katika Chelsea tunamshukuru Jose kwa mchango wake mkubwa tangu
aliporejea kama kocha kiangazi cha 2013. Makombe yake matatu ya
ubingwa wa Ligi Kuu, Kombe la FA na Ngao ya Hisani pamoja na makombe
matatu ya Kombe la Ligi katika misimu miwili vinamfanya kuwa kocha
aliyefanikiwa zaidi katika historia yetu ya miaka 110.
“Lakini Jose na bodi wamekubaliana kwamba matokeo si mazuri msimu huu
na wanaamini kwamba kilicho bora kwa kila upande ni kuachana. Klabu
wanapenda kuweka wazi kwamba Jose anaondoka kukiwa na uhusiano mzuri
na atabaki mtu aliyependwa sana, kuheshimiwa na muhimu kwa Chelsea.
“Ameacha alama kubwa Stamford Bridge na England na siku zote
anakaribishwa Stamford Bridge. Klabu sasa inajielekeza kuhakikisha
kwamba kikosi chetu chenye vipaji vingi kinafika pale panapotakiwa.
Hatutazungumzia suala hili tena hadi uteuzi wa kocha mpya
utakapofanywa,” ilisomeka taarifa ya Chelsea.
No comments:
Post a Comment