Rais John Magufuli amemalizia kujaza nafasi za uteuzi wa mawaziri na naibu waziri alizobakiza wakati akitangaza Baraza la Mawaziri la kwanza la Serikali ya Awamu ya Tano.
Katika taarifa iliyotolewa jana usiku na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu, walioteuliwa ni Profesa Jumanne Maghembe ambaye anakuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Philip Mpango kuwa Waziri wa Fedha na Mipango, Mhandisi Gerson Lwenge kuwa Waziri wa Maji na Umwagiliaji na Dk Joyce Ndalichako kuwa Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi.
Katika uteuzi huo, Rais Magufuli amefanya mabadiliko madogo ya Baraza hilo kwa kumhamisha Profesa Makame Mbarawa kutoka Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwenda Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.
Pia, amemteua Hamad Masauni kuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi.
Mawaziri wapya
Kabla ya uteuzi huo, Profesa Maghembe ambaye ni Mbunge wa Mwanga, alikuwa Waziri wa Maji katika Serikali iliyopita akiwa pia amewahi kuongoza wizara hiyo ya maliasili. Nyingine alizowahi kuongoza ni Kazi na Ajira na Elimu.
Mhandisi Lwenge ambaye pia ni Mbunge wa Njombe Magharibi, alikuwa Naibu Waziri wa Ujenzi akifanya kazi chini ya Dk Magufuli katika Serikali iliyopita.
Dk Mpango ambaye pia ameteuliwa kuwa mbunge, hivi karibuni aliteuliwa na Dk Magufuli kuwa kaimu Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), baada ya kumsimamisha kazi, Rished Bade kutokana na kashfa ya upotevu wa makontena katika Bandari ya Dar es Salaam.
Kama ilivyokuwa kwa Dk Mpango, Dk Ndalichako ambaye pia ameteuliwa kuwa mbunge aliwahi kuwa Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Taifa (Necta).
Maoni ya wadau
Akizungumzia uteuzi huo, Mwenyekiti wa Chama cha NCCR-Mageuzi, James Mbatia alisema kitendo cha Rais Magufuli kumhamishia wizara nyingine Profesa Mbarawa kunadhihirisha jinsi alivyokosa utulivu katika uteuzi.
Alisema ili nchi iweze kusonga mbele, inahitaji iwe na mfumo imara wa utawala ambao hauwezi kupatikana kama nchi haitakuwa na Katiba Mpya, kanuni na taratibu nzuri.
“Mawaziri wameteuliwa Desemba 10 na kuapishwa siku mbili baadaye. Leo (jana) ni siku ya 13 tangu wateuliwe tayari waziri mmoja amehamishwa wizara.”
“Dk Magufuli akitaka kuongoza nchi arudi katika msingi wa kubadili mfumo. Kasi ya mabadiliko ya dunia hatuwezi kwenda nayo sambamba kama tutaendelea kuwa na mfumo mbovu,” alisema Mbatia.
Profesa wa Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM), Kitila Mkumbo alisema kama kuna jambo Dk Magufuli amepatia, ni kumteua Dk Ndalichako.
“Ndalichako ni mzoefu na amekuwa katika sekta ya elimu kwa muda mrefu sana. Wizara hii imepata mtu sahihi na mwerevu maana kwa muda mrefu imekuwa ikipata watu ambao hawakuwa makini,” alisema.
Mhadhiri wa UDSM, Richard Mbunda aliungana na Mbatia, lakini akisisitiza kuwa uteuzi wa Rais unaonyesha jinsi CCM inavyokosa watu anaoweza kwenda na kasi yake.
“Ukitizama utabaini kuwa ameteua watu kuwa wabunge na kuwapa wizara nyeti. Hii inaonyesha kuwa ndani ya CCM kwa sasa wanakosekana watu ambao Dk Magufuli anawahitaji, kwa maana ya wachapakazi na watakaokwenda na kasi yake,” alisema.
Mbunda alipongeza uteuzi wa Dk Ndalichako kutokana na uzoefu wake katika sekta ya elimu.
Bosi mpya TRA
Kutokana na uteuzi wa Dk Mpango, Rais Magufuli amemteua Alphayo Kidata kuwa Kaimu Kamishna Mkuu wa TRA. Kabla ya uteuzi huo, Kidata alikuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
No comments:
Post a Comment