Baadhi ya watendaji wa Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI) wakimsilikiza Katibu Mkuu wa ofisi ambaye hayupo pichani.
Na Magreth Kinabo – maelezo
SERIKALI imewataka watendaji wa Mamlaka za Serikali za Mitaa nchini kuhakikisha kwamba wanafanyakazi kwa uadilifu weledi wa taaluma zao na kufuata sheria zilizopo katika kusimimia suala la usafi wa mazingira, likiwemo la kudhibiti biashara holela, gereji bubu,uegeshaji wa magari holela.
Pamoja na hayo wasimamie, upigaji holela wa muziki katika vilabu, baa na kumbi zaidi ya saa zilizopangwa na kuzuia bodaboda zinazosafirisha abiria hadi maeneo ya miji katikati, pia kuzuia ujenzi holela.
Kauli hiyo imetolewa leo na Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI), Jumanne Sagini wakati akizungumza na watendaji mbalimbali wa ofisi hiyo katika mkutano wa kikazi uliofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Karimjee, jijini Dar es Salaam ambapo lengo kuu lilikuwa ni kutoa maelekezo ya utendaji kazi kama ilivyoagizwa na Waziri Mkuu Majaliwa Kassim Majaliwa.
Akizungumzia kuhusu suala la usafi wa mazingira kufuatia ziara iliyofanyika hivi karibuni imeonekana kuwa na changamoto mbalimbali alisema;
“Kazi zetu haziendi vizuri kwa sababu hatusimamii sheria zilizopo ndio kumekuwa na malalamiko katika utendaji wa kazi zetu, mfano katika suala la gharama za usimamizi wa usafi wa mazingira ni kubwa . Lakini kinachofanyika ni kweli kinalinganishwa na gharama hizi?” alihoji Katibu Mkuu huyo.
Akitolea mifano gharama zinazotumika katika suala hilo, kwa kipindi cha mwaka wa fedha wa 2014/2015 alisema kwa upande wa manispaa ya Kindondoni wanatumia Sh. bilioni 2.6, Ilala ni Sh. bilioni 2.6, wakati Temeke wanatumia Sh. bilioni 1.2 .
“Kilichobainika ni kwamba mikataba ya watu wanaojishughulisha na usimamizi wa usafi wa mazingira ni ya mwaka mmoja na wanaopewa mikataba hiyo ni watu ambao hawana uwezo wa kutosha wa kutekeleza jukumu hilo.
“ Ama watu wasio na uwezo ama mnaofahamiana nao. Au kampuni zenye mahusiano na baadhi ya watumishi wa mamlaka za serikali za mitaa au wenye uhusiano na viongozi wenu, Jiepusheni na kuwapa watu hawa kwa sababu kutokana na hali hiyo hamtaweza kukabiliana nao. Kama kuna kiongozi ambaye mmepatia nafasi hii lazima athibitishe kuwa na uwezo. Na kama pia ni miongoni mwenu hakikisheni kuwa ni mtu mwenye uwezo. Kazi zetu haziendi vizuri kwa sababu ya nasaba au viongozi wenu,” alisisitiza Katibu Mkuu huyo, huku akisema lazima wabadilike na kuangalia kama hawana uwezo wajitoe au wafukuzwe.
Aliongeza kwamba katika suala hilo kumekuwa na migongano ya watumishi wa halmashauri ambao wanatakiwa kufanya kazi kama timu; mfano maafisa afya, mazingira na usafishaji, lakini akasema wanaonana kama maadui.
“ Hawa wangepaswa kufanya kazi kwa kushirikiana ,lakini ni maadui kwa sababu ya maslahi … hili ni lenu wakurugenzi kwani hata watoto wako wakisambaratika ni lazima huwaketishe chini ili mambo yaende, asiyekubali unamwajibisha,” alisema.
Sagini alisema watendaji hao , wote ni wadau wa usafi, hivyo wanapaswa kufanya kazi kwa ushirikiano, hivyo aliwataka wapeane mikono katika kikao hicho, ambapo walifanya hivyo ikiwa ni hatua ya kuonesha ushirikiano.
Pia alisema watu wanaosafirisha bidhaa za vyakula kwa kutumia majani ya migomba au matenga wasiruhusiwe kufanya hivyo wapewa muda wa wiki moja au mbili kutumia utaratibu mwingine.
Aliwataka pia watendaji mbalimbali wa TAMISEMI kuwa na ushirikishwaji katika ngazi za chini kwenye halmashauri kwa kuwa haliko vizuri.
Sagini alisema ni vizuri kukawekwa mfumo wa TAMISEMI wa kushirikisha ngazi za chini kama ilivyo kwa mjumbe wa nyumba kumi kwenye masuala ya vyama.
“ Ni lazima tuingie katika mfumo huu wa kuwa na watendaji wa kaya 30 ambao watakuwa chini ya TAMISEMI . Suala hili lina faida ya ulinzi na usalama na kuwatambua wageni… tunaangalia jinsi ya kulitekeleza,” alisema.
Aliwataka wakurugenzi wasikae maofisini kwenye madawati bali watembelee maeneo mbalimbali ili kutatua kero za wananchi na kuangalia mipangilio ya miji na majiji.
Katika suala hilo la usafi wa mazingira alisema mtu mwenye uwezo wa kusafisha jiji liwe safi apewe nafasi huku akisisitiza suala la kushirikisha sekta binafsi ni muhimu katika mambo mbalimbali likiwemo la ujengaji wa maegesho ya magari, ambapo sasa yanahitajika kwa ajili ya mradi wa mabasi yaendayo haraka(DART).
“ Kwenye eneo hili la DART lazima mbadilike tunataka barabara za DART ziwe nyeupe yaani watu wasifanye biashara,” alisisitiza huku akitaka kuanzia Jumatatu wiki ijayo yatekelezwe.
Aliwataka watu wanaohusika na vyombo vya usafiri na usafirishaji kutovunja sheria, akatolea mfano boda boda.
No comments:
Post a Comment