MAKAMPUNI 15 yaliyokwepa kodi baada ya kutorosha makontena yao, yamejisalimisha Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), lakini yameshindwa kulipa kodi ndani ya siku saba za msamaha wa Rais John Magufuli.
Kodi inayodaiwa kwa kampuni hizo ni Sh bilioni 3.75, hivyo watachukuliwa hatua za kisheria kwa kukwepa kulipa kodi, ikiwa ni pamoja na kufikishwa mahakamani.
Kaimu Kamishna Mkuu wa TRA, Dk Philip Mpango alisema hayo jana wakati akielezea makusanyo ya kodi ya makontena yaliyoondolewa katika bandari kavu ya Azam, kinyume cha sheria pamoja na kumalizika kwa siku saba alizotoa Rais Magufuli kwa wafanyabiashara hao kulipa kodi waliyokwepa, bila kuchukuliwa hatua nyingine za kisheria.
Dk Mpango alisema siku hizo saba zimefikia kikomo juzi, hivyo hatua kali za kisheria kwa wafanyabiashara ambao hawakulipa kodi katika kipindi hicho zinafuata hivyo wasubiri cha moto.
“Tumewasihi waje kulipa kwani huruma ya Rais sasa imeisha... tulifanya uhakiki na kuthibitisha kuwa kampuni hizo zipo. Wamekuja kulalamika lakini hakika hakuna atakayesamehewa kulipa na sasa tunafuata mkondo wa sheria ili kuwafikisha mahakamani,” alisisitiza.
No comments:
Post a Comment