Na Editor
16th December 2015
16th December 2015
Tanzania leo itafahamu hatma yake ya kama itapokea msaada wa fedha kutoka Shirika la Changamoto za Milenia la Marekani (MCC).
Bodi ya MCC inatarajiwa kukutana leo mjini Washington, Marekani ambapo pamoja na kuijadili Tanzania, inatazamiwa kujadili nchi nyingine zinazoendelea.
Kikao hicho kitaamua nchi za kupewa fedha hizo za kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo baada ya kukidhi vigezo.
Tanzania inasubiri kiasi cha dola milioni 472 (sawa na Shilingi trilioni moja) kwa ajili ya kufanya shughuli mbalimbali za maendeleo.
Hata hivyo, nchi yetu imejikuta njia panda kutokana suala la Zanzibar ambalo lilikumbushwa na uongozi wa MCC.
MCC baada ya kikao chake cha mwezi uliopita, ilionya kuwa itakuwa ngumu kwa Tanzania kupata fedha hizo ikiwa suala la Zanzibar halitakuwa limepatiwa ufumbuzi.
Pia, tukio la kukamatwa kwa watu mbalimbali kwa makosa ya mitandao wakihusishwa na ukusanyaji na ujumlishaji wa matokeo ya Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 25, mwaka huu.
MCC lilisema inahusisha na mambo hayo na utawala bora na suala la uhuru wa kujieleza na kuitaka Tanzania kushughulikia masuala hayo kama inataka ipate fedha za MCC.
Hata hivyo, Katibu Mkuu Kiongozi, Ombeni Sefue alikaririwa na gazeti hili juzi akieleza kuwa anaamini Tanzania itapata fedha hizo kwa kuwa suala la Zanzibar linashughulikiwa na la wahalifu wa mitandaoni liko mahakamani.
Tunaiomba serikali iongeze jitihada za kuutatua mgogoro wa Zanzibar kwani kwa kiasi kikubwa unaitia doa nchi yetu kwenye medani ya kimataifa.
Tanzania ni miongoni mwa mataifa yanayosifika duniani kwa kudumisha amani na utulivu miongoni mwa raia wake.
Ndiyo maana mara nyingi imehusishwa na jitihada mbalimbali za kutatua migogoro mbalimbali ya kimataifa ikiwamo ya Burundi, Sudan Kusini, Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Wengi wanajiuliza; imekuwaje mgogoro wa Zanzibar umeshindikana kutatuliwa?
Suala hili halijaanza leo kwani kumbukumbu zinaonyesha tangu miaka ya 1950 na 1960 wakati wa enzi ile ya vyama kama vya ASP, ZPPP na ZNP.
Tangu kurudi tena kwa mfumo wa vyama vingi katika chaguzi zote kuanzia ule wa mwaka 1995 hadi huu uliyopita, kila mara kumekuwa kukiibuka mgogoro kati ya vyama vya CCM na CUF.
Mgogoro wa safari hii uliibuka baada ya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar, Jecha Salim Jecha, kuamua kufuta matokeo ya uchaguzi wa Zanzibar.
Suala hili tayari limeanza kuiathiri Tanzania katika medani ya kimataifa, lakini pia hata kwa maisha ya wananchi wa Zanzibar.
Ni kwa msingi huo, tunashauri wanasiasa wa Zanzibar waelewe kuwa mgogoro huu kwa kiasi kikubwa umeanza kuiumiza Tanzania.
Wanasiasa wanaohusika na mgogoro huu wanapaswa kutanguliza maslahi mapana ya taifa wakati wakiushughulikia.
Shilingi trilioni moja ni nyingi na hasa kwa nchi yetu katika kipindi hiki inahitaji fedha za kutekeleza miradi ya maendeleo.
Ikumbukwe kuwa fedha hizi zilitakiwa kuekelekezwa kwenye masuala ya kusambaza umeme vijijini.
Mbali ya suala ya Zanzibar, lakini pia la watuhumiwa wa masuala ya mitandaoni wakihusishwa na ukusanyaji matokeo ya Uchaguzi Mkuu.
Tunafahamu kuwa suala hili liko mahakamani, lakini kwa suala la Zanzibar tunaomba ziongezwe jitihada za kuutatua mgogoro huu.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment