Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison G. Mwakyembe (Mb) amesema Serikali imepokea kwa masikitiko taarifa ya kifo cha msanii nguli wa filamu nchini Bw. Amri Athumani maarufu kama King Majuto kilichotokea jana usiku katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Dar es Salaam.
Aidha, Dkt. Mwakyembe amepokea salamu za rambirambi kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa kuondokewa na msanii huyo mkongwe katika tasnia ya filamu nchini.
Waziri Mwakyembe amemshukuru sana Mhe. Rais kwa ukaribu alionao na wanasanaa kwa ujumla wao na kwa kufuatilia kwa karibu matibabu ya King Majuto ndani na nje ya nchi.
"Serikali imekuwa ikishirikiana kwa ukaribu na familia ya King Majuto tangu wakati wa kumuuguza na kumpeleka nchini India kupata matibabu zaidi. Tutaendelea kuwa karibu na familia yake katika kipindi hiki kigumu cha msiba", amesisitiza Dkt.Mwakyembe.
Marehemu King Majuto alianza kazi ya uigizaji zaidi ya miongo minne iliyopita hadi anafikwa na mauti King Majuto alikuwa akiendelea na kazi yake katika tasnia ya filamu.
No comments:
Post a Comment