RAIA wa Burundi, Salumoni Msigara (21), amehukumiwa kwenda jela miaka miwili kwa kosa la kuingia nchini na kuishi bila kibali maalumu kutoka Idara ya Uhamiaji.
Hukumu hiyo ilitolewa juzi na Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga, Ushindi Swalo, baada ya Msigara kukiri kutenda kosa hilo.
Hakimu Swalo alisema kuwa mtuhumiwa ataanza kutumikia adhabu hiyo mara moja, ili liwe fundisho kwa watu wengine wenye tabia kama ya kuingia nchini na kuweka makazi ya kudumu bila kibali.
Awali, mwendesha Mashtaka wa Jeshi la Polisi, Sada Adam, alidai kuwa Msigara alikamatwa Agosti 2, mwaka huu majira ya alfajiri maeneo ya kituo kikuu cha mabasi Kahama yaendayo mikoani bila kuwa na kibali kinachomruhusu kuwapo nchini.
Sada aliendelea kudai kuwa katika shauri hilo la jinai namba 277/2018 Msigara ametenda kosa hilo kinyume cha kifungu namba 45, kikisomwa na kifungu namba 2 cha sheria ya uhamiaji namba 7 sura ya 54 kilichofanyiwa marejeo mwaka 2016.
No comments:
Post a Comment