Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila amesema ameachia uenyekiti wa CCM Mkoa wa Iringa kwa maelezo kuwa ameambiwa achague nafasi moja.
Ametoa kauli hiyo jana Jumamosi Agosti 25, 2018 wakati akizungumza na wafanyabiashara wa soko la Sido mjini Mbeya akiwa sambamba na maofisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Chalamila alilazimika kuweka bayana jambo hilo baada ya mfanyabiashara, Mohamed Miraji kumuuliza swali juu ya kauli za baadhi ya viongozi wanaosema kuwa maendeleo katika eneo fulani yanaletwa na CCM wakati wapo wanaotoa kodi na si wafuasi wa chama chochote cha siasa, kutaka Watanzania kushikamana.
Katika majibu yake Chalamila amesema, “Analozungumza ndugu Miraji ni jambo la msingi. Mimi kweli ni mwanasiasa, ni mwenyekiti wa CCM mkoa wa Iringa lakini Mbeya ni mkuu wa Mkoa.”
“Ila kule (Iringa) lazima nitaachia tu hakuna namna kwa sababu nimeambiwa nichague kitu kimoja. Sasa na wao wananiambia nichague kitu kimoja, ukuu wa mkoa na uenyekiti wa chama wanategemea nitaenda wapi?”
Amesisitiza, “Jamaa (Miraji) amezungumza pointi kubwa sana kwamba wakati mwingine kwa sababu labda Mbeya ni ya Chadema au kwa sababu kata fulani ni ya CCM maendeleo hayafiki kwa sababu ni upinzani.”
“Nasema hivi wakati mwingine sisi wanasiasa tuna vikauli ambavyo huwa vinachukiza lakini mvione kama ni vikauli vya Yanga na Simba, vikauli vya Manchester United na Real Madrid, vikauli vya Wasafwa na Wanyakyusa au mvione kama vikauli vya Wahehe na Wabena, lakini tusihamishie mihemko hiyo kwenye maendeleo.”
No comments:
Post a Comment