NA Erick Pekepeke
KIKOSI cha Mo Bejaia cha nchini Algeria kilichoifunga Yanga bao 1-0 katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, kimezidi kujiimarisha baada ya kusajili kiungo matata kutoka Ufaransa mwenye uwezo mkubwa ndani ya dimba kama ilivyo kwa Thaban Kamusoko na huenda akawepo mchezo wa marudiano Uwanja wa Taifa.
Waarabu hao wamemsajili, Youcef Touati, kutoka katika klabu ya
Champly inayoshiriki Ligi Daraja la Tatu nchini Ufaransa kwa mkataba wa miaka mitatu kuwasaidia katika michuano mbalimbali ikiwamo ya kimataifa.
Kiungo huyo ambaye ana umri wa miaka 27, amezaliwa katika kitongoji cha Saint Denis nchini Ufaransa akichezea timu mbalimbali nchini humo na sasa anahamishia makali yake katika klabu hiyo ya Mo Bejaia.
Kiungo huyo ni mkali wa kupiga pasi za mwisho na pia ni mzuri linapokuja suala la kuzuia mashambulizi ya timu pinzani lakini pia anao uwezo mkubwa wa kufunga kama ilivyo kwa Mzimbabwe wa Yanga, Thaban Kamusoko.
Timu ambazo amepitia kiungo huyo ni Red Star ya Ligi Daraja la Tatu nchini Ufaransa ambapo aliichezea michezo 27 akifunga mabao mawili msimu wa 2011/12, kabla ya kujinga na FC Istre ya Ligi Daraja la Pili akicheza michezo 11 lakini hakufanikiwa kufunga.
Msimu wa 2013/14 alijiunga na FC Tour ya Ligi Daraja la Pili na alicheza michezo sita tu kabla ya kujiunga na Epinal ya Ligi Daraja la Tatu akifunga mabao mawili katika michezo 21 na baadaye kuhamia Champly aliyoichezea michezo 20 na kufunga mabao matatu.
Kikosi hicho mwishoni mwa wiki ijayo kitakutana na TP Mazembe katika mfululizo wa michuano hiyo ya Kombe la Shirikisho huku ikijiandaa kuja nchini Tanzania kumenyana na Yanga mchezo wa marudiano.
No comments:
Post a Comment