Jana simulizi hii iliishia wakati mteja aliponiambia nichukue Sh5,500 zilizobaki kwenye Sh10,000 baada ya kuniagiza nimletee bia moja na viroba viwili. Hii ilikuwa siku ya kwanza tangu nianze kazi ya uhudumu baa. Sasa endelea...
Nikiwa nimekaa akanifuata Matroni Rukia. Akanionyesha baba moja aliyekuwa amekaa kaunta akinywa na kuniomba nikaonane naye.
“Unamuona yule baba pale aliyevaa shati la kijivu?” anauliza huku akinionyesha na kisha ananiambia: “Nenda kaonane naye.”
Naenda kwa mwanamume huyo na baada ya kufika ananishika mashavu yangu huku akisema: “Sasa umeniona mtoto mzuri?
“Wenzako hawajakwambia taratibu za hapa?”
Nikamjibu: “Hawajaniambia, kwani kuna taratibu zipi?”
Akacheka na kunijibu akisema: “Kwani matroni alivyokwambia uje kuniona hajakwambia?”
Nikamjibu kuwa hakuniambia kitu zaidi ya kunielekeza nije kukuona, nikijua pengine unahitaji kuhudumiwa kinywaji.
Anacheka kisha ananiuliza: “Wewe ni raia wa Tanzania kweli? Nikamjibu ndiyo. Akasema: “Hapana. Wewe utakuwa Mkenya, hata lafudhi yako inaonekana wewe ni Mkenya na mwonekano wako pia. Sema ukweli kabla hatujakuitia uhamiaji. Sikiliza umeshapata bwana?”
Nami nikamuuliza kwa mshangao nikisema: “Bwana!”
“Ndiyo” akanijibu nami nikamwambia kuwa bado sijampata.
“Sasa nataka mimi niwe mume wako,” akasema.
“Hapa huwa kuna taratibu kama hawajakwambia wenzako. Ukiwa hapa lazima uwe na mwanaume wako ambaye atakutunza wewe siku zote unapokuwa hapa.”
Akaniambia kuwa anataka niwe mke wake kuanzia muda huo na nifanye shughuli zangu zote, nikimaliza atakuja kunichukua kwenda kulala naye nyumba ya wageni.
Nikaamua kumuacha na kuondoka. Nilipofika sehemu niliyokuwa nimeketi, matroni akaniuliza: “Eeh! niambie kakwambiaje?”
Nikamuelezea jinsi yule baba alivyoniambia na matroni akacheka kisha akaniambia kuwa ndivyo wanavyoishi kwenye baa hiyo.
“Wenzako wote wana waume zao wanaowatunza,” akasema matroni.
Nikabaki kinywa wazi aliposema wanaume wa aina hiyo ndiyo wanaowaleta wateja, yaani ni madalali wao. Hivyo, malipo yao ni kutembea na wahudumu wa baa hiyo na kuwapa ofa ya bia.
“Huwa wanaitwa ‘Sinaga Hela’,” akasema matroni.
Nikamuuliza itakuwaje kama sijampenda. Je, utanilazimisha?
“Hiyo ni lazima, haina cha kupenda wala kutopenda. Hao ndiyo wanaweza wakachagua uendelee kufanya kazi baa hii au uondoke kulingana na utakavyoweza kumhudumia mmojawapo kitandani na hasa anapokuwa amelewa.
“Pia, mwanaume huyo atakapokuja na wateja wake, atakuchagua wewe kwenda kuwahudumia. Siyo kwa vinywaji pekee bali hata huduma ya ngono kama watakuhitaji na yeye atatoa ruhusa na kiasi cha fedha utakacholipwa utakapotoa huduma hiyo kwa wateja anaowaleta.
“Kama utaweza kuwahudumia vyema, wateja hao wakavutika kurudi tena, hiyo ndiyo heshima yako na unaweza kupandishwa cheo,” akaniambia matroni.
Hakika haya ni ‘mashikoro mageni’ kama wajisemeavyo Wasukuma.
Lakini naambiwa na matroni huyo kwamba ukiwa na mwanaume huyo, huruhusiwi kuwa na mwingine na ikitokea mwanaume mwingine anataka kutoka na wewe, yule ambaye wamekuchagulia anatakiwa kulipia fedha kaunta Sh5,000, lakini haruhusiwi kuwa na uhusiano wa muda mrefu wa kimapenzi na wewe.
Ikitokea umempenda mwanaume tofauti na huyo uliyetafutiwa au yule anayekulipia Sh5,000 kaunta, itabidi iwe siri na bosi wako asijue, lakini ni lazima umwambie matroni wako na huyo ndiye atakufichia siri.
Hata unapotoka kwenda kustarehe na mwanaume huyo, ni lazima uache chochote kwa matroni.
Hakika ukistaajabu ya Mussa basi utayaona ya Firauni. Baada ya kupokea maelezo hayo kutoka kwa matroni, anaondoka na kuniacha nikiwa nimekaa peke yangu huku nikitafakari jambo hilo.
Mara anakuja mhudumu mwenzangu niliyemfahamu kwa jina la Neema. Ananiuliza sababu za kukaa peke yangu. Nikamjibu kuwa kuna baba mmoja kaniambia niwe mke wake.
“Mimi sipendi, halafu hata sijampenda. Kwanza mwanaume mwenyewe mzee, halafu matroni anasema ni lazima niwe naye kwa kuwa ndiyo taratibu za hapa.”
Neema akanicheka akisema, “ndiyo hivyo mama. Kwani wewe hujawahi kufanya kazi hizi? Ukija kufanya kazi ya baa, lazima ukubaliane na kila kinachokuja mbele yako”.
“Hapa kila mtu ana mwanaume wake. Siku akikuhitaji, bosi au matroni anakwambia mapema unafanya kazi zako zote ukimaliza unaondoka,” anasema.
“Wao ndiyo wanaotuhudumia. Hata mimi ninaye. Ni mtu mzima ana mke na watoto.”
Wakati nikiongea na Neema, mara anaitwa kuhudumia mteja mwingine na hivyo kuniacha nikiwa nimekaa peke yangu. Baada ya muda mfupi, anakuja rafiki yangu Sharifa na ananiambia nimpe mchapo.
“Shoga yangu nimekuona unaongea na baba pale, vipi ndo bwana nini?” Ananiuliza.
Nikamjibu, “hapana.”
“Mwanaume mwenyewe mzee mimi nitampeleka wapi?” nikasema na kusababisha acheke.
“Acha ujinga wewe. Mbona mimi ninaye mtu mzima ana pesa! Hapa anasubiri Mfungo wa Ramadhani uishe akanipangishie chumba,” anasema Sharifa huku akipepesa macho na kubinua midomo yake.
“Pia, nina bwana wangu mwingine ambaye anamjua matroni peke yake ana pesa balaaa.”
Sharifa ni msichana wa miaka 16 na anasema ameshatoa mimba mara mbili.
“Rafiki yangu, kwa hiyo wewe una wanaume wangapi hapo ulipo?” nikamuuliza.
“Loh! shoga yangu hapa mjini. Siwezi nikawahesabu, ila wengi ni wale ambao nawatumia kuwachuna pesa tu. Wanaweza kufika kumi, lakini wapo wale wa dharura, hao ni wengi sijui hata idadi,” anasema binti huyo ambaye wenzake wanamuita “digidigi”.
Msichana huyu ni mjanja machoni, ni mdogo lakini wanasema ni hatari na wenzake wanamchukia kwa sababu anawachukulia wanaume wao.
“Yule baba ana pesa, mkubali,” ananishauri.
Wakati tukiendelea na maongezi, wale wateja niliowahudumia mzinga wa konyagi wananiita. Nilipoenda, wakaniambia wanataka nikae nao.
“Mbona umetutenga? Unakaa na wenzako tu unatuacha. Hebu njoo ukae hapa, ninaketi kisha mmoja wa wateja hao aliyejiita ni ‘usalama wa taifa’, akaanza kunitongoza akitaka niondoke naye usiku huo.
Ninamkatalia, jambo lililomfanya apayuke “sijawahi kumtongoza mwanamke wa baa akanikatalia nakushangaa wewe. Fredy (meneja wa baa) kakutoa wapi? Mbona hujakaa kama wenzako?”
Aliendelea kubembeleza anataka niwe ‘mtu wake’ kwa siku hiyo tu na kwamba atanipa fedha.
“Unasikia mama. Kwanza najua hujala, naomba nikununulie chakula ule baadaye tunaondoka,” anasema baba huyo.
Wakati nikiendelea kuzungumza na ‘mwanausalama’ huyo, Sharifa ananiita na kuniuliza nachoelezwa na huyo mwanaume.
Nilipomweleza, akasema huyo mwanaume hana pesa.
“Fanya hivi, kama kakwambia anakununulia chakula, wewe kubali. Mlie hivyo viela vyake, uachane naye,” anasema Sharifa.
Nikarudi kukaa na huyo baba ambaye alimuita mhudumu wa chakula na kumwagiza atengeneze nyama choma na ndizi. Baada ya saa moja, chakula kikaletwa na tukala wote tuliokuwa kwenye meza hiyo, akiwamo Sharifa.
Baada ya kula, Neema akarudi na kuniita pembeni kukaa naye.
“Vipi sasa? Tunakaribia kufunga, utaondoka na yule baba? Nikamjibu hapana na kwamba sijamuona muda mrefu.
“Atakuwepo kama amesharuhusiwa na bosi uondoke naye, lazima utaondoka naye. Labda cha kufanya, jifanye unaumwa ndiyo itakuwa ponapona yako.”
Nikaamua kufanya kama alivyoniambia Neema. Wakati huo ilikuwa imetimia saa 5.00 usiku. Kaunta kulishafungwa na kubakia ukumbi wa baa ambako walikaa watu wachache wakitazama mpira.
Mara baba anayejiita ‘usalama wa taifa’ akanifuata na kunisisitiza niondoke naye, lakini nikakataa mbele ya Neema. Baadaye wahudumu tukaondoka kwenda ndani kulala.
Tukiwa ndani au gheto, matroni akaniuliza vipi mbona hujaenda?” akimaanisha sijaenda kulala na mwanaume niliyekabidhiwa.
Nikamwambia kuwa naumwa ugonjwa wa kikubwa, akaniuliza tena kama niliongea naye na kukubaliana naye kwamba nisiende alikotaka.
Nikamweleza kuwa sikumwambia, jibu lililomfanya matroni aende nje kumweleza, kisha akarudi na kusema: “Mtu mwenyewe keshalewa, hata hajitambui. Wewe lala tu mtamalizana kesho.”
ITAENDELEA KESHO
No comments:
Post a Comment