Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi Meja Jenerali Projest Rwegasira amemsimamisha kazi Mhasibu Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Frank Charles Msaki kutokana na makosa ya kufanya malipo hewa yaani kulipa posho ya chakula kwa watu ambao si askari.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka Wizarani hapo ambayo nakala tumeipata, Mhasibu Mkuu huyo Bw. Frank Msaki anasimamishwa kazi kwa kufanya malipo ya kiasi cha sh. 305,820,000 kama posho ya chakula kwa watu ambao sio askari kwa kipindi cha kuanzia mwaka wa fedha 2013/2014 hadi 2015/2016.
Meja Jenerali Rwegasira amesema kwa mujibu wa Sheria, Kanuni na Taratibu za Kijeshi anayetakiwa kulipwa posho ya chakula yaani ‘ration allowance’ ni askari peke yake na si mtu mwingine yeyote yule.
Meja Jenerali Rwegasira amesema anamsimisha kazi Mhasibu Mkuu huyo tangu leo tarehe 9 Julai, 2016 ili kupisha uchunguzi ufanyike juu ya tuhuma zinazomkabili.
Katibu Mkuu huyo amesema baada ya jalada la uchunguzi kufunguliwa na Ukaguzi Maalumu kufanywa na Mkaguzi wa Ndani wa Jeshi la Polisi imebainika kuwa mbinu mbalimbali zimetumika ili kufanikisha malipo hayo hewa.
No comments:
Post a Comment