Na Erick Mlelwa
WAKATI zikiwapo taarifa kuwa Vital’O ya Burundi imekamilisha usajili wake huku likiwamo jina la Laudit Mavugo, mashabiki wa Simba wanaweza wakaendelea kufurahi kwani straika huyo inasemekana amefichwa na Wekundu hao wa Msimbazi.
Taarifa kutoka Simba zinadai kuwa
straika huyo amefichwa moja ya hoteli kubwa nchini Burundi huku wakimhudumia kila kitu na muda wowote wanamleta nchini ili kumalizana naye.
Simba wamekuwa wakimfukuzia mkali huyo wa mabao tangu msimu uliopita lakini ilishindikana baada ya klabu yake ya Vital’O kumwekea ngumu na sasa Wekundu hao wa Msimbazi wanataka kufanya umafia.
Simba na Mavugo walifikia makubaliano lakini Vital’O wakaweka dau kubwa lililowashinda Wekundu hao wa Msimbazi wakaamua kurudisha majeshi nyuma ingawa sasa wanataka kufanya kweli.
Kigogo mmoja wa Simba aliliambia DIMBA Jumatano kuwa licha ya taarifa kuenea kwamba straika huyo yupo kwenye usajili wa Vital’O, mashabiki wa Wekundu hao wa Msimbazi wasiwe na wasiwasi kwani kila kitu kinakwenda vizuri.
“Ni kweli kwamba kuna taarifa za Vital’O kumjumuisha kwenye usajili wao lakini hilo lisiwape presha mashabiki wetu kwani tunafanya mipango yetu kimya kimya,” alisema kigogo huyo.
DIMBA lilikwenda mbali na kumtafuta straika huyo ili kuzungumzia maisha yake ya msimu ujao ambapo alisema yupo nchini kwao Burundi akisubiri kutumiwa tiketi na Simba aje Tanzania.
“Nilishamaliza mkataba na Vital’O na sasa nipo huru, nimefanya mazungumzo na Simba na ninachosubiri ni wao wanitumie tikieti. Ni kweli kwamba bado Vital’O wanataka kunisainisha mkataba mpya lakini siyafikia makubaliano nao,” alisema.
Mwenyekiti wa kamati ya usajili ya Simba, Zachari Hanspope ambaye kwa sasa yuko Marekani, amewataka mashabiki na wanachama wa Simba kutokuwa na hofu juu ya ujio wa Mavugo kwa vile mtu aliyemwachia jukumu hilo yuko makini.
No comments:
Post a Comment