NJOMBE
WAKULIMA wa zao la viazi mviringo mkoani Njombe, wameiomba serikali
iwasaidia kuwakabiri walanguzi wa mazao mkoani humo ambao bado wanatumia
ujazo wa Lumbesa – kwa madai kuwa ujazo huo unadumaza uchumi wa mkulima.
Wakulima hao kutoka katika kijiji cha Ibumila Wilayani Njombe, wamesema
wanalazimika kuuza Viazi mviringo kwa ujazo mkubwa wa Lumbesa – kutokana na
wanunuzi kutaka ujazo huo na hivyo mkulima kushindwa kumudu gharama za
pembejeo za kisasa.
John Mwambuji amesema kuna umuhimu kwa serikali kudhibiti ujazo wa Lumbesa
kwa nchi nzima, badala ya mkoa mmoja pekee wa Njombe, ili wanunuzi wasipate
upenyo wa kukimbilia mikoa mingine isiyo na udhiti wa ujazo wa Lumbesa, kwamadai
kuwa zoezi hilo limekuwa likiwasababishia hasara baada ya wanunuzi kutonunua Viazi Njombe.
Salvius Kawogo – afisa kilimo wa kijiji cha IbumilaWilayani Njombe- amesema
changamoto ya Lumbesa inatokana na tatizo la upatikanaji wa soko, ambapo
mkulima hulazimika kuuza shilingi elfu 37, 500 gunia moja lenye ujazo wa
debe 8 zenye zaidi ya kilo 150.
Saimon Chatanda afisa kilimo wa Wilaya ya Njombe, amesema tatizo la Lumbesa
kwa wakulima wa Viazi Mviringo lipo na linatokana na ugumu wa namna ya
kudhibiti ujazo wa Lumbesa, changamoto inayotokana na uwepo wa soko huria.
Aidha Chatanda amesema kila wanapodhibiti Lumbesa wakulima wao hukosa soko
kwakuwa wanunuzi hukimbilia maeneo yasiyo na udhibitio huo wa Lumbesa- huku
akiwataka wakulima kuwa na umoja ili kukabiriana na changamoto hiyo ya
Lumbesa, ikiwa pamoja na kutumia mizani badala ya ujazo.
Hata hivyo Owekisha Kwigizile afisa mradi wa uzalishaji na usambazaji wa
mbegu bora za Viazi Mviringo mkoani Njombe- “SAGCOT” chini ya ubia wa
kampuni ya Yara, Syng’enta na Mtanga foods- wanatoa mafunzo ya kilimo bora
cha Viazi Mviringo ikiwa pamoja na kuwatafutia Soko la uhakika ili
kuwaepusha wakulima na walanguzi wanaonunua Viazi kwa ujazo wa Lumbesa
No comments:
Post a Comment