KOCHA wa timu ya soka ya Al Ahly, Martin Jol, amesema uimara wa safu ya ulinzi ya Yanga ilikuwa kikwazo kibwa kwao wasiibuke na ushindi juzi. Timu hizo ziliumana katika mchezo wa kwanza Raundi ya Pili Ligi ya Mabingwa Afrika na kumalizika kwa sare ya bao 1-1 katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Al Ahly walitangulia kupata bao la mapema mfungaji akiwa Amri Gamal dakika ya 11 kabla ya Yanga kusawazisha dakika ya 18 baada ya beki wa Ahly, Ahmed Hegazy kujifunga katika harakati za kuokoa.
Akizungumza baada ya mchezo huo, Jol alisema ulikuwa mzuri vijana wake walicheza vizuri na kutengeneza nafasi nyingi za mabao, lakini kikwazo ilikuwa ni umaliziaji baada ya kazi nzuri ya mabeki wa Yanga.
“Mchezo ulikuwa mzuri na mgumu ingawa safu ya ulinzi ilifanya kazi nzuri kwa upande wa wenyeji, lakini kwa ujumla mchezo ulikuwa mzuri. Yanga ni timu inayocheza mpira mzuri wenye pasi nyingi na hii inatulazimu katika mchezo wa marudiano kutumia mipira mirefu ili tuweze kupata ushindi hata wa mabao 2-0, “ alisema Jol.
Kwa upande wake, kocha wa Yanga Hans Pluijm, alisema mchezo ulikuwa mgumu kwa sababu walikutana na timu bora Afrika ambayo inaundwa na wachezaji wenye uzoefu na vipaji vya hali ya juu.
Alisema ameona upungufu wa wapinzani wao na wanajipanga kwa ajili ya mchezo wa marudiano nchini Misri na kuahidi watajitahidi kupambana ili kupata bao la ugenini kama walivyofanya wapinzani Al Ahly.
No comments:
Post a Comment