Mechi za mkumbo wa pili Kundi C katika michuano ya kombe la taifa bingwa Afrika kwa wachezaji wa ligi za ndani zimemalizika kwa klabu zote kutoshana nguvu.
Nigeria walitangulia kwa kutoka sare ya 1-1 na Tunisia mjini Kigali.
Bao la Nigeria lilitingwa wavuni na Elvis Chikatara dakika ya 51.
Tunisia walihakikisha wanaondoka na alama moja baada ya kusawazisha kupitia Ahmed Akaichi dakika ya 69. Akaichi alikuwa ametumbukiza mpira kimiani kwa kichwa dakika ya kwanza lakini alikuwa ameotea.
Kwenye mechi ya pili, Issa Moussa alifungia Niger bao la kwanza nao Guinea wakapata lao kupitia Alseny Camara.
Ammadou Issa, aliyekuwa ameingia uwanjani kama nguvu mpya, aliweka Niger kifua mbele dakika ya 49.
Aboubacar Bangoura hata hivyo alikomboa bao hilo na mambo yakasalia hivyo hadi kipenga cha mwisho kilipopulizwa.
Kwa sasa Nigeria wanaongoza kundi hilo na alama nne, Tunisia na Guinea wakifuata wakiwa na alama mbili kila mmoja, nao Niger inavuta mkia ikiwa na alama moja pekee.
Mechi za mwisho Kundi C zitachezwa Jumanne wiki ijayo ambapo Nigeria watacheza dhidi ya Guinea nao Tunisia wacheze dhidi ya Niger.
No comments:
Post a Comment