RAIS John Magufuli ametoa mwito kwa Watanzania kumuombea ili aendelee kuwashughulikia wote wanaofanya ubadhirifu wa fedha za umma kupitia kampeni yake ya kutumbua majipu.
“Nataka niwahakikishieni kuwa nitaendelea kutumbua majipu yote mpaka yaishe, na naomba mniombee ili kazi hii ya kutumbua majipu ifanyike kwa mafanikio,” alisema Dk Magufuli.
Alitoa kauli hiyo wakati alipokuwa akizungumza na wananchi katika mikoa ya Kilimanjaro na Arusha jana, alipotua kwa ziara ya kikazi ikiwa ni ya kwanza kwao tangu achaguliwe kushika wadhifa huo Novemba 5, mwaka jana.
Dk Magufuli aliwasili mkoani Arusha, ambako kesho atatunuku Kamisheni kwa maofisa wanafunzi wa kundi la 57/15 katika Chuo cha Mafunzo ya Kijeshi (TMA) Monduli mkoani hapa.
Rais Magufuli aliwasili mjini Arusha akitokea Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), alikotua kwa ndege akitokea jijini Dar es Salaam na kupokewa na mamia ya wananchi. Akiwa uwanjani hapo, Rais Magufuli aliwashukuru wananchi kwa mapokezi makubwa aliyoyapata na aliwaeleza kuwa uchaguzi umekwisha, kilichobaki ni kazi tu.
“Nawashukuru sana ndugu wananchi kwa mapokezi haya makubwa, naomba kuwahakikishia kuwa uchaguzi umekwisha na sasa kilichobaki ni kuchapa kazi tu,” alisema Rais Magufuli.
Akiwa njiani kutoka KIA, Rais Magufuli alisimamishwa na wananchi wa njiapanda ya KIA, Kikatiti, Usa River, Tengeru na Mount Meru mjini Arusha ambako huko kote pamoja na kusisitiza kuwa uchaguzi umekwisha na kilichobaki ni kuchapa kazi, aliwahakikishia kuwa hatawaangusha.
Aidha, Rais Magufuli alisema tayari serikali imeanza kutoa fedha kwa ajili ya kugharimia elimu ya msingi na sekondari baada ya kufuta ada na alionya kuwa watumishi wa umma hususani wakuu wa shule watakaothubutu kufanya ubadhirifu wa fedha hizo watashughulikiwa.
Alisema yote aliyoyaahidi kwa wananchi wa mkoa wa Arusha na Watanzania kwa ujumla, ikiwemo ujenzi wa barabara za Arusha, kulipa fidia za wananchi na kufuta ada ya shule za msingi na sekondari yanatekelezwa.
Rais Magufuli alisisitiza kuwa serikali yake haitawabagua Watanzania kwa dini zao wala makabila yao na wala haitawabagua kwa misingi ya vyama vyao na kanda zao. Aliwataka Watanzania wote kuiweka mbele Tanzania na kushirikiana kuiendeleza.
No comments:
Post a Comment