Nigeria wameshindwa kufuzu kwa fainali za mataifa ya Afrika (Africa Cup of Nations) mwaka 2017 nchini Gabon baada ya kuchezea kichapo cha bao 1-0 mbele ya Misri kwenye mchezo wa kundi G mechi iliyopigwa Jumanne usiku.
Wakiwa wamebakiza mchezo mmoja mkononi, huku kinara wa kundi ndiye anayefuzu kwenye michuano hiyo, Nigeria haina nafasi tena ya kwenda Gabon. Endapo Nigeria itashinda mchezo wake wa mwisho dhidi ya Tanzania itafikisha pointi 5 wakati tayari Misri inapointi saba mkononi ikiongoza kundi G.
Goli la Ramadan Sobhy la dakika ya 65 limeiweka Misri kwenye nafasi nzuri ya kufuzu kucheza fainali za mataifa ya Afrika mwaka 2017.
Tanzania itaialika Misri mwezi June na Misri watajihakikishia kukata tiketi ya Gabon kwa matokeo yoyote isipokuwa kama watapoteza mchezo huo kwa magoli 3-0.
Nigeria ilitwaa ubingwa wa Cup of Nations mwaka 2013 lakini sasa wameshindwa kufuzu kwenye michuano hiyo kwa mara ya pili mfululizo
Nigeria ilijitahidi kutafuta goli la kusawazisha na ilikaribia kufanya hivyo pale winga wa West Ham Victor Moses alipoachia shuti kali dakika ya 84 likagonga mwamba.
Mchezo huo uliopigwa Alexandira ulikuwa wa kufa na kupona kwa Nigeria baada ya Chad kujitoa kwenye kundi G kuwania kufuzu kushiriki fainali hizo kwa sababu ya hali ngumu ya kiuchumi na kusababisha matokeo yote ya awali yaliyoihusisha timu hiyo kufutwa.
Hatua hiyo ya Chad kujitoa imepelekea kubaki timu tatu kwenye kundi G na kwa mujibu wa kanuni za CAF timu itakayoongoza kundi ndiyo itafuzu moja kwa moja kushiriki fainali zijazo.
Misri ina pointi saba huku ikiwa na mechi moja mkononi dhidi ya Tanzania iliyo nafasi ya mwisho kwenye kundi ikiwa na pointi moja lakini inamichezo miwili ya kucheza.
Ili Tanzania iweze kufuzu kucheza fainali zitakazofanyika Gabon mwaka 2017, inahitaji ushindi usiopungua magoli 3-0 dhidi ya Misri sawa na yale ambayo ilifungwa na Misri mwezi June mwaka uliopita timu hizo zilipokutana kwasababu matokeo ya head-to-head yatatumika kuamua ni timu ipi itafuzu endapo timu zitamaliza zikiwa na pointi sawa kwenye kundi husika.
Wakati huohuo Tanzania itahitaji ushindi mwingine kwenye mchezo wao wa mwisho dhidi ya Nigeria mwezi September mwaka huu.
No comments:
Post a Comment