Muhammad Yussuf
Katika Gazeti la NIPASHE toleo la Jumaane tarehe 20 Desemba 2016, kulichapishwa makala yenye kichwa cha maneno “CCM yarudisha kivingine staili ya uvuaji magamba”. Pamoja na mambo mengine, Mwandishi wa makala hiyo,Thobias Mwanakatwe, aliandika kama hivi:
“CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimesema matajiri wenye mikono michafu inayohusika na rushwa na dhuluma, wakae kando na chama hicho kwa kuwa kimeanza safari ya
mageuzi ili kusimamia misingi ya uadilifu, haki, uaminifu na uwajibikaji.
Katibu wa Halmashauri Kuu Taifa (NEC), Itikadi na Uenezi, Humprey Polepole, aliyasema hayo juzi wakati akihojiwa na kituo kimoja cha runinga kuhusu mambo mbalimbali yanayoendelea ndani ya CCM likiwamo suala la mabadiliko yaliyofanywa hivi karibuni na vikao vya juu vya chama hicho.
“Kuwa tajiri si dhambi na si kwamba CCM inafukuza matajiri, hapana. Tatizo letu kama CCM katika mwelekeo mpya, mtizamo mpya na mageuzi yanayofanyika, hatuhitaji kuwa na aina ya matajiri wanaojipatia utajiri wao kwa hila, kwa rushwa na kwa dhulma.
Polepole alisema tajiri aliyepata utajiri kwa hila, halipi kodi. “CCM inajiweka kando naye tunaielekeza serikali kuwashughulikia watu wa aina hiyo na wanapokosea, wawajibishe kwa mujibu wa Katiba, sheria na taratibu za nchi,” alisema Polepole. “Ukijiona wewe ni tajiri na mikono yako ni michafu kwa maana ya kuwa na makando kando ya kukosa uaminifu, hulipi kodi, ukae mbali na CCM,” alisema.
Alisema CCM haiwachukii wafanyabiashara, bali inawachukia watu wasio waadilifu na wenye mikono michafu inayohusika na rushwa na dhulma na kwamba ni wakati sasa kwa viongozi ndani ya CCM waishi kwenye mwenendo bora.
Aliongeza kuwa CCM ijayo itafika mahali ambapo kama mtu ana mambo mengi kwenye biashara yake kiasi kwamba hana muda wa kuhudumia chama na wanachama, ni bora akachagua moja. Alisema CCM imeanza safari ya mageuzi makubwa ambayo faida yake itakuwa ni kwa wanachama na wananchi kwa ujumla kwa kusimamia misingi ya uadilifu, haki uaminifu, uwajibikaji.
MAONI: Nakubaliana kabisa na hoja ya ndugu yangu Hamphrey Polepole kuhusiana na wana-CCM waliokosa maadili mazuri, uadilifu na uwajibikaji. Mimi ningelienda mbali zaidi kwa kupendekeza kuwa Wana-CCM wafanya biashara wasiruhusiwe kugombea nafasi yoyote ile katika chama na serikali. Wachague siasa au kufanya biashara; hawawezi kufanya yote wakati mmoja. Cha kusikitisha zaidi ni kuona jinsi ambavyo katika siku za karibuni wafanya biashara wanavyoingia katika siasa wakati wa uchaguzi ili wapate fursa ya kugombea nafasi mbali mbali, kama vile ubunge na uwakilishi.
Kusema kweli, wana-CCM wa aina hii hawana kiu ya kuwatumikia wananchi isipokuwa uchu wa kugombea madaraka tu. Na wengi wao, baada ya kushinda katika chaguzi, hawachangii chochote katika mijadala inayoendelea bungeni au barazani. Hukaa kimya mpaka uchaguzi mwengine unapowadia. La muhimu zaidi kwao ni kupata paspoti za kibalozi pamoja na heshima na fursa nyingine zinazoambatana na nyadhifa zao ili biashara zao zishamiri vizuri zaidi. Wana-CCM kama hawa hawafai hata kidogo kuwaongoza wananchi.
No comments:
Post a Comment