LIGI Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL), imeendelea kutimua vumbi kwenye viwanja mbalimbali nchini huku ikishuhudiwa Wekundu wa Msimbazi, Simba, wakizidi kung’ara huku watani zao (Yanga) wakizidi kupunguzwa kasi jana.
Simba wakiwa kwenye dimba la Taifa jijini Dar es Salaam, waliendelea kutoa vipigo vya mbwa mwizi, baada ya kuwapigisha kwata Maafande wa Mgambo JKT ya Handeni Tanga kwa mabao 5-1.
Ushindi huo wa vijana wa Jackson Mayanja, umekuja siku tano ikitoka kutoa dozi ya mabao 4-0 kwa African Sports kwenye uwanja huo huo.
Katika mchezo wa jana, Simba ilianza mahesabu dakika ya 5 kwa bao la Hamis Kiiza akiitendea haki pasi ya Ibrahim Ajib.
Dakika ya 14, Mwamuzi Emmanuel Mwandembwa wa Arusha aliamuru penalti baada ya beki mmoja wa Mgambo kuunawa mpira katika eneo la hatari, lakini Kiiza alishindwa kuitendea haki.
Kiungo Mwinyi Kazimoto, aliifungia Simba bao la pili dakika ya 28 kwa shuti la mbali.
Mshambuliaji anayekuja juu kwa kasi, Ajib, dakika 42 aliwanyanyua vitini mashabiki wa Simba baada ya kufunga bao safi kwa kuwachambua mabeki watatu na kipa wao Mudathir Khamis, kisha kuunyunyiza mpira kambani.
Hadi mapumziko Simba walitoka uwanjani kifua mbele kwa mabao 3-0 huku wakikosa nafasi nyingi za kufunga.
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi huku Mgambo wakilishambulia lango la Simba huku wakishindwa kufunga baada ya mashambulizi yao mengi kuishia mikononi mwa Kipa Agban Vincent .
Dakika ya 77, mtokea benchi Dan Lyanga aliyeingia akichukua nafasi ya Ajib, aliifungia Simba bao la nne kwa shuti kali nje ya 18 lililomshinda kipa Khamis kabla ya Kiiza kukamilisha mahesabu kwa bao la tano dakika ya 83.
Watoto wa ‘Mchawi Mweusi’ Bakari Shime, Mgambo, walijipatia bao la kufutia machozi dakika ya 88 likifungwa na Full Maganga akimalizia pasi ya Ally Nassoro.
Simba: Vincent Angban, Ramadhani Kessi, Abdi Banda, Hassan Isihaka, Juuko Murshid, Xavi Majabvi, Mwinyi Kazimoto, Jonas Mkude, Hamis Kiiza, Ibrahim Ajibu, Haji Ugando.
Mgambo JKT: Mudathir Khamis, Bakari Mtama, Salim Mlima, Salim Kipaga, Ramadhan Malima, Henry Chacha, Sunday Magoja, Mohamed Samata, Full Maganga, Ally Nassoro na Aziz Gilla.
Tanzania Prisons 2-2 Yanga
Tanzania Prisons: Beno Kakolanya, Laurian Mpalile, Benjamin Asukile, James Mwasote, Nurdin Chona, Jumanne Elfadhil, Lambert Sabiyanka, Fred Chudu, Mohamed Mkopi, Jeremiah Juma na Leonce Mutalemwa.
Yanga: Deo Munishi, Abdul Juma, Oscar Joshua, Vincent Bosou, Mbuyu Twite, Juma Makapu, Deus Kaseke, Haruna Niyonzima, Amissi Tambwe, Donald Ngoma na Isafou Boubacar.
No comments:
Post a Comment