RAIS
Dkt. John Magufuli ameagiza sh. milioni 308 zilizotengwa kwa ajili ya
Maadhimisho ya Siku ya Kumbukumbu ya Mashujaa, zitumike kuboresha
miundombinu ya barabara jijini Dodoma.
Ametaja
miundombinu hiyo ni pamoja na taa za kuongezea magari katika barabara
ya Kisasa na taa za barabarani kwenye barabara mpya ya Emmaus-African
Dream yenye urefu wa kilomita 1.4, ambayo kwa sasa inajengwa kwa kiwango
cha lami.
Taarifa
hiyo imetolewa na Waziri Mkuu jana (Ijumaa, Juni 29, 2018), wakati
akizindua kituo cha polisi kinachohamishika katika hafla iliyofanyika
eneo la Kisasa, jijini Dodoma. Kila ifikapo Julai 25 ya kila mwaka
Tanzania huadhimisha siku ya mashujaa.
“Sasa
kutokana na msongamano uliopo ambao unaweza kusababisha ajali,
Mheshimiwa Rais na Amiri Jeshi Mkuu, Dkt. Magufuli ameamua fedha zote
zilizoandaliwa kwa ajili ya maadhimisho hayo zitumike kuboresha
barabara,” amesema
Waziri
Mkuu amesema Rais Dkt Magufuli anawataka Watanzania wote waadhimishe
siku hiyo ya kumbukumbu ya mashujaa kwa kufanya usafi katika maeneo
yaliyo jirani na makazi yao pamoja na yale ambayo wamezikwa mashujaa
ikiwa ni njia ya kuwaenzi.
Kufuatia uamuzi huo, Waziri Mkuu amewaagiza Wakuu wa Mkoa waratibu zoezi hilo kwenye maeneo yao.
Katika
hatua nyingine, Waziri Mkuu ameliagizaJeshi la Polisi lianze kujikita
kwenye matumizi ya mifumo ya kiulinzi ya kielektroniki yaaniCity
Surveillance Sytemsili limudu kudhibiti hali ya sasa ya uhalifu.
Amesema
kutokana na kuwepo kwa mapinduzi makubwa ya kiteknolojia duniani,
hususani kwenye nyanja mbalimbali ikiwemo eneo la ulinzi wa raia na mali
zao, hivyo ni wakati muafaka sasa kwa Jeshi la Polisi lianze kutumia
teknolojia za kisasa.
“Usimikaji
wa mifumo hiyo si tu utasaidia kupunguza uhalifu na kuongeza usalama wa
wananchi na mali zao lakini pia utaongeza imani kwa wafanyabiashara na
watalii wanaotembelea nchi yetu,” amesema.
Pia
Waziri Mkuu amewasisitiza wakazi wa eneo hilo kukitumia vizuri kituo
hicho ni kwa kupeleka taarifa za uhalifu. “Aidha, naomba niwasisitize
kituo hiki ni cha muda, hivyo uongozi wa eneo hili ni lazima uje na
mkakati wa kupata kituo cha kudumu,”.
Ufunguzi
wa kituo hicho ambacho ni kati ya vituo vitano vilivyogharimu sh.
milioni 250 vilivyotolewa na Benki ya Equity mkoani Dodoma; umehudhuriwa
na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni.
No comments:
Post a Comment