Mwanasiasa aliyejitangaza kuwa kiongozi wa vuguvugu la pingamizi dhidi ya serikali nchini Kenya NRM Miguna Miguna alikamatwa siku ya Ijumaa alfajiri, muda mfupi baada ya
kupiga kamsa kufuatia uvamizi wa polisi katika nyumba yake iliopo katika makaazi ya Runda jijini Nairobi.
Mkurugenzi wa kitengo cha ujasusi nchini Kenya George Kinoti alithibitisha kwamba bwana Miguna alikamatwa kwa kutoa kiapo kinyume na sheria mbali na kuwa mwanachama wa vuguvugu la NRM lililopigwa marufuku linalohisishwa na muungano wa Nasa.
''Bwana Miguna alitangaza hadharani kwamba yeye ndio jenerali wa vuguvugu hilo, ambalo tayari limetangazwa kuwa kundi haramu.Wakati alipotangaza hadharani kulikuwa na notisi ya gazeti rasmi la serikali iliotolewa na waziri''.
''Tutamuachaje sisi ni maafisa wa polisi'', alisema Kinoti.
''Pia alisema kwamba atawaongoza watu kuchoma picha za rais Uhuru aliyechaguliwa kidemokrasia.Sasa munatarajia nini kutoka kwetu''?.
''Pia alikiri kwamba ni yeye aliyeongoza kiapo hicho''.
- Kiongozi aliyekamatwa kwa kuhusishwa na kiapo cha Raila aachiliwa
- Raila 'aapishwa' kuwa 'rais wa wananchi' Kenya
- Sherehe ya kumuapisha Odinga imeahirishwa
- Viongozi waliowahi kuapishwa kama Odinga barani Afrika
Duru za maafisa wa polisi zimethibitisha kuwa bwana Miguna alipelekwa katika kituo cha polisi cha Kiambu kabla ya kuondolewa na kupelekwa eneo lisilojulikana.
Mapema bwana Miguna alimwambia muhariri wa gazeti la Nation kwamba maafisa wa polisi walivamia nyumba yake mapema alfajiri na kuipekuapekua .
Wakili huyo ambaye alikuwa kiungo muhimu katika kumuapisha kiongozi wa Nasa Raila Odinga siku ya Jumanne katika uwanja wa Uhuru Park jijini Nairobi alithibitisha uvamizi huo katika ujumbe uliotumwa saa moja na robo alfajiri Ijumaa.
''Maafisa wa polisi walitumia bomu kuvunja na kuingia katika nyumba yangu. Siwezi kuzungumza katika simu hivi sasa. Wamepekua nyumba yangu'', alisema.
''Wengine wamejificha nje ya nyumba yangu wakitumai nitatoka ili waweze kunipiga risasi na kudai kwamba kulikuwa na ufyatulianaji wa risasi. Sitoki ng'o''.
Majirani walisema kuwa magari kadhaa yalikuwa katika nyumba ya Miguna mapema saa kumi na mbili alfajiri, lakini magari hayo baadaye yakaondoka.
Wafuasi wa Miguna walikuwa wameanza kujaa nje ya nyumba yake na baada ya dakika tano maafisa wa polisi walidaiwa kurusha vitoa machozi ili kuwatawanya.
Wafuasi hao walitoroka na kutazama kwa mbali huku magari ya polisi yaliombeba Miguna yakiondoka.
Baada ya maafisa wa polisi kuondoka , waandishi wa habari waliweza kuingia ndani, na hakukuwa na ishara yoyote ya Miguna huku nyumba hiyo ikiwachwa bila mtu.
No comments:
Post a Comment