WAZIRI MKUU Majaliwa Kassim Majaliwa amesema Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kuhakikisha kila kinachokusanywa kama mapato ya nchi kinatumika kwa maslahi ya Watanzania wote na si kwa manufaa ya wachache.
Ametoa kauli hiyo leo mchana (Jumapili, Novemba 29, 2015) wakati akifunga maadhimisho ya miaka 20 ya Dayosisi ya Pwani ya Kanisa la African Inland Church Tanzania (AICT) kwenye ukumbi wa PTA, viwanja vya Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam.
“Serikali imeanza kukabiliana na upotevu wa mapato ya Serikali na kuepuka matumizi yasiyo ya lazima ya fedha za umma. Nia yetu ni kuhakikisha kila kinachopaswa kukusanywa kama mapato ya nchi, kikusanywe na kitumike kwa masuala ya msingi kwa ustawi wa Watanzania wote na si kwa watu wachache,” alisema.
Akifunga maadhimisho hayo kwa niaba ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli, Waziri Mkuu alisema Serikali imedhamiria kupambana na maovu yote na kuondoa kero zinazowaumiza wananchi wa kawaida. “Wako watu wanaoamini kwamba hatuwezi, nawaomba waondoe hiyo dhana. Wako watu wanaodhani kwamba kwamba utawala huu ni wa watu wapole, nao pia waondoe hiyo dhana,” alisema huku akishangiliwa na mamia ya waumini waliohudhuria sherehe hizo zilizoanza Novemba 27, 2015.
“Tunawaomba Watanzania wote mtuunge mkono kwenye vita hii na mtuwezeshe kuifanya kazi hiyo. Tunaomba waumini wote mtuombee katika sala zenu za kila siku ili tuweze kuongoza kwa haki na kuwaletea Watanzania wote maendeleo,” aliongeza.
Akinukuu kitabu cha Mithali sura ya 29 mstari wa pili, Waziri Mkuu alisema: “Wenye haki wakiwa na amri, watu hufurahi, bali mwovu atawalapo, watu huugua. Mtuombee viongozi wenu tuwe waadilifu na wenye kutenda haki. Nasi tutaendelea kuwa waadilifu ili watu wetu wasigue,” alisema.
Aliwataka viongozi wa kanisa hilo waendelee kuisaidia Serikali katika kujenga kundi la watu wenye maadili mema ili walisaidie Taifa kuwa na watu waadilifu na hivyo kupunguza kero nyingi zinazoikabili jamii.
Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na waumini wa kanisa la hilo kutoka mikoa mbalimbali, Askofu Mkuu wa Kanisa la AICT, Askofu Silas Kezakubi alisema Kanisa hilo litaendelea kumuombea Rais Dkt Magufuli na viongozi wenzake ili wawe na afya njema, wawe na hekima na kuahidi kwamba wataendelea kuwaweka chini ya ulinzi wa Mungu siku zote.
Alisema wao kama kanisa wanaamini kwamba Serikali ya awamu ya tano ina nia ya kuwatumikia wananchi kwa bidii na uadilifu lakini akasisitiza kuwa siri ya bidii na uadilifu inapatikana kwenye neno la Mungu.
Akisoma risala ya kanisa hilo, Askofu wa AICT Dayosisi ya Kibaha, Askofu Charles Salalah alisema kanisa halina budi kushirikiana na Serikali kwa sababu wote wanawahudumia watu walewale isipokuwa katika malengo tofauti.
Alisema kanisa hilo linahubiri maadili mema na bidii katika kazi kwa vile linaamini kuwa maendeleo hayadondoki kutoka juu wala hayaoti kama uyoga bali yanapatikana kwa watu kufanya kazi.
Akisisitiza kuhusu uadilifu, aliwataka wazazi kudumisha ndoa zao ili watoto wapate malezi mema kutoka kwa baba na mama na kwamba baba na mama wasipokaa vizuri, watoto hawawezi kuwa waadilifu.
“Wazazi tunao wajibu wa kupanda mbegu bora ya uzalendo kwa watoto wetu. Endapo tutapanda mbegu mbaya ya kuwagawa watoto wetu kwa itikadi tofauti, ni lazima tujue kuwa tutavuna tunachopanda.”
“Tukumbuke kuwa tunalo Taifa moja tu la Tanzania. Hata kama watoto wetu watakuwa na upenzi na vyama vyao, ni lazima tuwalee katika misingi ili wakue wakijua Taifa letu ni moja tu. Ndiyo maana tunaweka mkazo kwenye familia kwa sababu maadili mema yanaanzia nyumbani,” alisisitiza.