Guterres ameahidi kufanya kazi na uongozi wa Trump ingawaje kumekuwepo na msuguano na atajaribu kushirikiana katika kuondoa "changamoto mbali mbali" ambazo Marekani na Umoja wa Mataifa zitakabiliana nazo siku za usoni.
Katibu Mkuu mpya wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres tayari ameshachukua madaraka ya
juu katika taasisi ya dunia Jumapili, baada ya Ban Ki Moon kumaliza muda wake Desemba 31 saa sita usiku.
Guterres, ambaye ni waziri mkuu wa zamani wa Ureno na aliyekuwa kamishna wa idara ya Umoja wa Mataifa ya kuhudumia wakimbizi, ameiambia taasisi hiyo ya dunia katika hotuba yake kuwa suala la namna ya kuwasaidia watu waliokumbwa na migogoro na vita lina uzito mkubwa moyoni mwake.
Aliongeza kuwa wananchi wasio na hatia wanaendelea kukabiliwa na nguvu za kikatili, wanauawa na kujeruhiwa, wanatobanduliwa katika makazi yao na kutumbukizwa katika ufukara. Alilalamika kuwa hata mahospitali na misafara ya misaada haiko salama tena kutokana na vita.
Guterres amewataka wafanyakazi wenzake Umoja wa Mataifa "kukubaliana katika azimio moja la pamoja la mwaka mpya: Hebu basi tukubaliane kwamba amani ndiyo kitu cha kwanza."
"Hili lionekane kutoka kwenye mshikamano wetu na upendo wetu katika maisha yetu ya kila siku na mazungumzo na kuheshimiana katika migawanyiko yetu ya kisiasa," alisema.
Guterres ameahidi kuwa ni mwenye kuiunganisha dunia wakati rais mteuli wa Marekani, Donald Trump ameeleza wasi wasi wake kuwa Umoja wa Mataifa haina mashiko.
Hata hivyo Guterres ameahidi kufanya kazi na uongozi wa Trump ingawaje kumekuwa na msuguano na atajaribu kushirikiana katika kuondoa "changamoto mbali mbali" ambazo Marekani na Umoja wa Mataifa watakabiliana nazo siku za usoni.
Ban, ambaye amemaliza muda wake amewaambia wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa katika hotuba yake ya mwisho aliyoitoa Ijumaa "anajivuna sana" kufanya kazi nao kwa miaka kumi iliyopita.
Amewasihi waweke vipaumbele vyao na kuendelea kufuata malengo yao ya juu ya mambo ya maendeleo endelevu, kama vile mabadiliko ya tabia nchi, kuwawezesha wanawake, kuwawezesha vijana na mambo mengi mengineyo.
No comments:
Post a Comment